Saturday, March 6, 2021

JINSI YA KUJIJENGEA BAHATI YA MAFANIKIO KWENYE MAISHA YAKO.

Watu wote ambao wanafikia mafanikio makubwa, huwa kuna bahati wanazokutana nazo kwenye safari yao ya mafanikio, japo siyo wote wanaoziona. Na pia bahati hizo haziwafuati kitandani wakiwa wamelala, badala yake wanakutana nazo wakati wanapambana.




Naval Ravikant anasema kuna aina kuu nne za bahati;

Aina ya kwanza ni bahati kipofu, hii ni pale mtu anapokutana na bahati ambayo hakuitegemea kabisa kwenye maisha yake. Mfano unatembea barabarani na kukutana na jiwe la dhahabu, hiyo ni bahati ambayo imekutokea tu, hakuna namna unaweza kujisifu umechangia kuipata.

Aina ya pili ya bahati ni ile inayotokana na mtu kuweka juhudi na ung’ang’anizi kwenye kile anachofanya. Hapa mtu anakuwa amechagua kufanya kitu, lakini anakutana na changamoto na vikwazo ambavyo hajui hata atavivukaje, lakini hakati tamaa, anaendelea kuweka juhudi na baadaye anakutana na fursa nzuri inayomwezesha kufanikiwa. Bahati hii inatengenezwa kwa sababu kama mtu angekata tamaa mapema, asingekutana nayo.

Aina ya tatu ni ile inayotokana na ujuzi maalumu, ambapo mtu unakuwa na uwezo wa kuona kitu ambacho wengine hawakioni. Kuna watu wanaona vitu ambavyo wakivifanyia kazi, vinawapa matokeo makubwa na kwa wengine inaonekana ni bahati. Bahati ya aina hii inaweza kutengenezwa, hasa kwa mtu kujipatia ujuzi ambao wengine hawana.

Aina ya nne ni pale unapojijenga sifa ya kipekee ambapo bahati inakufuata mwenyewe. Aina hii ya bahati ni ngumu kwa sababu mtu unakuwa umejijengea sifa fulani ambayo kwa sasa unaweza usione matumizi yake, lakini siku moja kikatokea kitu ambacho hakuna anayeweza kukifanya, ila wewe kwa sifa uliyonayo, ndiye pekee unayeweza kufanya na hapo ukapata fursa kubwa. Kujenga aina hii ya nne ya bahati, jua ni kitu gani unacho ambacho wengine hawana, kisha kiendeleze na jijengee sifa kwenye kitu hicho. Na ipo siku usiyoijua, watu watakutafuta uwasaidie kwenye kitu hicho na watakuwa tayari kukupa chochote unachotaka.

Jinsi ya kujijengea bahati.

Ukiachana na aina ya kwanza ya bahati ambayo inatokea bila wewe kujua, aina tatu za bahati unaweza kujijengea kwenye maisha yako.

Na unaweza kufanya hivyo kupitia kujijengea sifa ya kipekee kupitia kile unachotaka kufanikiwa.

Na sifa ya kwanza muhimu kabisa unayopaswa kujijengea ni kuwa mtu wa kufanya na siyo tu kupanga na kuahidi.

Wengi kwenye maisha huwa wanaweka malengo makubwa, wanakuwa kabia na mipango ya kufikia malengo hayo, lakini inapokuja kwenye kuchukua hatua, ndipo wanaofanikiwa na wanaishindwa wanapotofautiana.

Wanaoshindwa huwa ni watu wa kutafuta sababu kwa nini hawawezi kufanya na hata wanapoanza ni rahisi kuahirisha.

Lakini wale wanaofanikiwa, wanaposema wanafanya, wanafanya kweli, ni watu wa matendo na siyo maneno pekee, siyo watu wa kutoa sababu, bali ni watu wa kutoa matokeo.

Hivyo kama unataka kujijengea bahati itakayokufikisha kwenye mafanikio, chagua eneo unalotaka kufanikiwa na chukua hatua kila siku. Siyo kupanga pekee, bali kuchukua hatua kila siku.

Kwa kuchukua hatua kila siku, unajiweka kwenye nafasi kubwa ya kukutana na bahati kuliko yule asiyechukua hatua kabisa au anayechukua hatua pale anapojisikia pekee.

Kufanya siyo rahisi, hasa kwa namna ambavyo wengi wamejijengea tabia kwenye maisha yao. Hivyo hii ni tabia unayopaswa kuweka juhudi kubwa kwenye kuijenga.

Kwa wengi, kufanya kila siku siyo kitu wanachoweza kujisimamia na wakakikamilisha.

No comments:

Post a Comment