Saturday, November 23, 2019

USISINGIZIE MTAJI TENA , KAMA HUJAINGIA KWENYE BIASHARA TATIZO SIYO MTAJI , BALI TATIZO NI WEWE.

Andrew Carnegie ambaye alikuwa mtu tajiri kuliko wote duniani enzi za uhai wake, aliwahi kuandika kitabu alichokiita GOSPEL OF WEALTH, kwa tafsiri rahisi ni INJILI YA UTAJIRI.

Katika injili yake hiyo, alieleza ni jinsi gani utajiri ni mzuri na njia pekee ya mtu kuisaidia jamii ni kuwa tajiri. Lakini pia alionesha ni jinsi gani ilivyo rahisi kufikia utajiri kama umeanzia kwenye umasikini kuliko kutokea kwenye utajiri.

Kikubwa zaidi ambacho Carnegie ametueleza kupitia kitabu chake hicho ni njia ya uhakika ya kuelekea kwenye utajiri ni kufanya biashara. Anasema ajira ni sehemu ya kuanzia, sehemu ya kujifunza na sehemu ya kutengeneza mtandao. Lakini utajiri mkubwa haupatikani kwenye ajira, bali kwenye biashara.

Andrew aliamini kama mtu angeweza kuanzisha na kuendesha vizuri biashara yake, angeweza kufanikiwa sana. Na yeye mwenyewe hiyo ndiyo njia aliyopita, alianza kama kibarua kwenye kampuni ya reli, na baadaye kuweza kuanzisha kampuni yake ya kufua vyuma ambayo ilimfikisha kwenye mafanikio makubwa.